Picha ya wasifu ya Brian Crowley, Mkurugenzi wa Matangazo ya Kimataifa na Uchunguzi wa Maudhui hapa Google.

Kulinda usalama wa watumiaji kwenye intaneti inayoonyesha matangazo


Kuanzia kusaidia biashara ndogondogo zipate wateja wapya hadi kuruhusu watu wengi wafikie taarifa, matangazo husaidia kuunga mkono intaneti kama tunavyofahamu leo. Google huchangia kwa kiasi kikubwa katika mfumo huu wa utangazaji dijitali. Je, inafanya nini kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama dhidi ya matangazo mabaya? Brian Crowley, Mkurugenzi wa Matangazo ya Kimataifa na Uchunguzi wa Maudhui hapa Google anajadili kuhusu watu, sera na michakato maalum ya kazi hii.

Tasnia ya utangazaji wa mtandaoni ni kubwa na inaendelea kukua, lakini ni nini kinasababisha kuwepo kwa 'tangazo baya'?


Matangazo mengi yanayoonekana mtandaoni yanafuata sheria zinazotumika za maudhui ya tangazo na zinachangia kuwa na mfumo salama wa utangazaji dijitali. Lakini pia kuna matangazo ambayo yanakusudia kukiuka kanuni hizi kwa kupotosha, kuwakilisha kwa njia ya uwongo au kutishia usalama wa watumiaji.

Matangazo haya tunayaita matangazo mabaya na yanahusisha nyanja mbalimbali za matatizo ya maudhui, kitu chochote katika matangazo haya ambacho kina maudhui yasiyofaa, kulaghai, kutangaza uuzaji wa bidhaa hatarishi.

Sera zinazotumika katika matangazo zinahusisha vipengele viwili vikuu. Hivi ni pamoja na kupiga marufuku aina fulani za bidhaa, huduma na maudhui yasionyeshwe kwenye matangazo na kudhibiti aina nyinginezo za bidhaa, huduma na maudhui.

Matangazo yenye maudhui yaliyopigwa marufuku yanaweza kuwa ni pamoja na maudhui ambayo yanakusudia kumlaghai mtumiaji au jambo fulani ambalo tunachukulia kuwa halifai kama vile maudhui yanayoonyesha ukatili kwa wanyama. Tabia ya aina hii ni hatarishi na hairuhusiwi katika mifumo yetu.

Maudhui yaliyozuiwa humaanisha kuwa tangazo linaruhusiwa kuonyeshwa kwenye huduma za Google, lakini kwa kufuata masharti. Tangazo hili linaweza kuwa tangazo la kamari au pombe ambalo haliwezi kuonyeshwa katika baadhi ya maeneo ya kijiografia kutokana na taratibu za kitamaduni au sababu za kisheria.

Ili kukupatia muhtasari wa hatua tulizochukua, mwaka 2021 tuliondoa matangazo mabaya bilioni 3.4 na kudhibiti mengine bilioni 5.7 kabla hayajaonyeshwa kwa watumiaji. Shughuli hii ni jambo la msingi katika dhamira ya Google na husaidia kuwalinda watu wasione maudhui yasiyofaa kwenye matangazo.

Je, ni nani anafanya uamuzi kuhusu sera hizi?


Hawa ni watu wa ajabu na wenye ari kutoka timu za Google za sera, bidhaa na vipengele vinavyoaminika ambao wanashughulikia kuunda hali salama ya utumiaji kwa watumiaji, watayarishi, wachapishaji na watangazaji. Kuleta hali salama ni jambo la msingi katika dhamira yao.

Na katika timu hii kubwa, tuna watu sehemu mbalimbali duniani waliojikita katika kuunda na kusasisha sera zetu za matangazo. Wanafanya kazi katika maeneo tofauti, wanazungumza lugha tofauti na hushughulikia mada mahususi ili kuhakikisha sera zetu zinaendana na mabadiliko ya tasnia ya matangazo. Uanuai huu hutusaidia kutathmini utofauti wa kitamaduni na kimaeneo na kubaini mianya ya mada wakati wa mchakato wa uundaji.

Lakini hatutegemei tu ujuzi wetu wa ndani, pia tunaomba ushauri nje ya Google, kama vile kwenye mashirika yanayoshughulikia usalama wa watoto na wataalamu wa matibabu. Wataalamu hawa hutusaidia kubaini mianya katika sera kutokana na ujuzi na uzoefu wao kwenye mada hizo, wakihakikisha sera zetu zinafaa na zinaweza kutekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Je, Google inakabiliana vipi na matatizo yanayojitokeza?


Kadiri intaneti inavyokua, tutaendelea kuona aina mpya za matangazo hatarishi yakionekana, ikiwa ni pamoja na matangazo ambayo yanatumia fursa ya matatizo ya kijamii kuwapotosha watumiaji au kulenga mambo mapya yanayovuma. Ni jambo ambalo mara zote tutaweka jitihada kukabiliana nalo na mnamo mwaka 2021 tulisasisha sera zaidi ya 30 ili kudhibiti hatari zinazojitokeza katika matangazo.

Mfano mmoja tuliouona katika nusu ya pili ya mwaka 2021 ulikuwa ni kuongezeka kwa matangazo ya ulaghai yanayotangaza sarafu ya dijitali. Kadiri sarafu ya dijitali ilivyowavutia wengi zaidi, watu wengi walikuwa wakitafuta mtandaoni ili kujifunza kuhusu bidhaa na kampuni dijitali. Katika hali hii, upya wa tasnia uliwasaidia watendaji wabaya kuwapotosha watumiaji katika maudhui yao ya tangazo kwa kuiga chapa ambazo tayari watu walizifahamu.

Kukabiliana na aina hizi za matangazo hatarishi ni muhimu sana na ukiukaji huu pekee umesababisha zaidi ya akaunti 136,000 kuzuiwa au kusimamishwa na zaidi ya akaunti milioni 2.1 kusimamishwa kutokana na uwakilishi wa uwongo au wizi wa data binafsi.

Miaka michache iliyopita tumeshuhudia matukio ya kipekee ulimwenguni. Je, matukio haya yalikuwa na athari gani katika usalama wa matangazo?


Matukio ya ulimwengu kama vile migogoro au harakati kubwa za kisiasa mara nyingi zinaanzisha mambo yanayovuma kwa watendaji wabaya wanaotafuta njia mpya za kuwapotosha watu mtandaoni. Matukio haya hutokea kwa haraka na tunahitaji kuchukua hatua upesi.

Katika kipindi cha mwanzo cha janga la COVID-19, tulishuhudia ongezeko la matumizi mabaya ya matangazo yanayoonyeshwa katika njia tofauti, hivyo tulihitaji kuwa wepesi na kushughulikia hali hii katika mchakato wote, kuanzia masasisho hadi utekelezaji wa sera. Katika miezi 12 ya mwanzo ya janga, tulizuia zaidi ya matangazo milioni 99 yanayohusiana na Covid, ikiwa ni pamoja na tiba za miujiza, barakoa za N95 kutokana na kupatikana kwa uchache na hata vipimo bandia vya dawa ya chanjo.

Matukio kama haya pia hufichua njia zingine za ukiukaji wa sera na matatizo mtandaoni ambayo si dhahiri. Kwa kawaida, tunaona ukiukaji huu katika kundi kubwa la watendaji wabaya wanaojaribu kutumia fursa ya mkanganyiko na hali ya shinikizo kama ambavyo janga linasababisha. Hivyo, visa vya Covid-19 vilipojitokeza tulitekeleza sera ambayo inazuia tabia kama vile kuongeza bei za bidhaa zinazohitajika kwa kiasi kikubwa kama vile vitakasa mikono, barakoa na bidhaa za karatasi.

Je, nichukue hatua gani ikiwa sivutiwi na tangazo na nisingependa kuliona tena?


Tunafahamu kwamba hata ikiwa tangazo halikiuki sera zetu, kunaweza kuwa na sababu nyinginezo zinazopelekea usipende kuliona.

Kituo changu cha Matangazo cha Google hukupatia njia rahisi ya kudhibiti matangazo unayoona kwenye huduma ya Tafuta na Google, YouTube na Gundua. Zana hii hukuruhusu udhibiti taarifa zinazotumika kuonyesha matangazo, ikiwa ni pamoja na taarifa zinazohusiana na Akaunti ya Google na tunachokadiria kuhusu mambo yanayokuvutia kulingana na shughuli za mtandaoni. Zinaweza pia kutumika kuweka mapendeleo ya hali ya tangazo kwa mtumiaji ili uone biashara nyingi zaidi uzipendazo na kudhibiti zile usizozipenda. Unaweza pia kufuta kabisa data ya shughuli inayohusiana na akaunti yako wakati wowote.

Uamuzi huu umefanyika kutokana na maoni ya watumiaji wetu walioomba udhibiti zaidi wa hali yao ya tangazo kwa mtumiaji. Uwazi na kuweka jitihada katika aina hizi za zana bado ni kipaumbele kwetu na tutaendelea kuunda vidhibiti vya watumiaji kwenye bidhaa zetu.

Je, watangazaji wanawezaje kujua sheria zinazotumika za maudhui ya tangazo?


Inafaa watangazaji na wachapishaji wafahamu kuhusu sera zetu za matangazo na jinsi tunavyozitekeleza, ndivyo mifumo hii itafanya kazi vizuri zaidi.

Mtangazaji anapounda tangazo au kampeni mpya, tunampatia taarifa kuhusu sera zetu katika mchakato mzima kupitia kituo chetu cha usaidizi. Maudhui mapya ya tangazo yanakaguliwa na ikiwa hayatimizi viwango vyetu vya sera tutamtaarifu mtangazaji kuhusu vipengele alivyokiuka na hatua anazoweza kuchukua. Mifumo hii hutusaidia kuhakikisha usalama wa matangazo kwa watumiaji kabla hayajachapishwa na kuwapatia wachapishaji mwongozo wa maudhui yanayofaa.

Je, ni hatua zipi zinachukuliwa kutekeleza sera hizi?


Idadi ya ushiriki wa kila siku na aina mbalimbali ya maudhui mtandaoni humaanisha kuwa hakuna njia moja mwafaka ya kuhakikisha utekelezaji wa sera.

Akili bandia ya kompyuta na mfumo wa mashine kujifunza ni muhimu katika kusaidia kupanga maudhui na kugundua ukiukaji katika kiwango kikubwa. Mifumo hii hufanya kazi na wahandisi wanaoshughulikia kuboresha bidhaa, wachanganuzi pamoja na wataalamu kubaini mambo mapya yanayovuma na watu wanaokagua ambao wanaweza kufanya uamuzi kuhusu hali husika. Ni mchakato wa maoni unaofanya timu na teknolojia zetu zifanye kazi pamoja kila wakati ili kuendelea kuboresha na kusasisha michakato yetu.

Tumeona ongezeko kubwa la matangazo mabaya tunayoondoa. Katika Ripoti ya Usalama wa Matangazo mwaka 2021 tulirekodi kuwa kati ya mwaka 2019 na 2021, idadi ya matangazo mabaya ambayo yaliondolewa yaliongezeka kutoka bilioni 2.7 hadi bilioni 3.4. Takwimu hizi zinaonyesha kukua kwa idadi ya watangazaji lakini pia kuboreshwa kwa utambuzi unaofanywa na mfumo wa mashine kujifunza na kupanuka kwa sera zetu katika kukabiliana na hatari zinazojitokeza. Ni mchakato unaoendelea na tutaendelea kuongeza juhudi katika jitihada hizi kila mwaka.

Sera yetu ya uthibitishaji wa utambulisho huhitaji baadhi ya watangazaji kwenye mifumo ya Google kukamilisha mpango wa uthibitishaji ili kuthibitisha utambulisho wao na mpango huu utaendelea kupanuliwa kadiri muda unavyosonga. Uthibitishaji huu huwapatia maelezo zaidi watumiaji kuhusu anayetangaza na huwasaidia kufanya uamuzi sahihi zaidi wanapotumia vidhibiti vyetu vya utangazaji.

Mara kwa mara tunatoa ripoti ambazo hutoa maarifa si tu kuhusu matokeo ya jitihada zetu za utekelezaji wa sera lakini pia kuhusu michakato yetu iliyofanyika ili kutekeleza sera. Mwaka 2021 ilitimia miaka kumi ya kuchapisha Ripoti ya Usalama ya Google Ads, ambayo inatoa muhtasari wa kazi tunayofanya kuzuia matumizi hasidi ya mifumo yetu ya matangazo, jinsi tunavyotekeleza sera zetu au kukagua maudhui yaliyoripotiwa kukiuka sheria za eneo husika.

Intaneti inayoonyesha matangazo humaanisha kila mtu anaweza kufikia taarifa muhimu. Mfumo huu unavyoendelea kukua, ndivyo wajibu wa Google kuwapatia watumiaji hali bora ya utumiaji katika mifumo yake unavyoongezeka. Ripoti yetu ya Usalama wa Matangazo inachapishwa kila mwaka na unaweza kusoma toleo kamili la 2021 hapa.

Uboreshaji wa usalama mtandaoni

Pata maelezo kuhusu jinsi tunavyohakikisha usalama wa watu wengi zaidi mtandaoni kuliko shirika lolote lingine duniani.

Pata maelezo zaidi