Kubuni faragha na usalama ambao unamfaa kila mtu
Kituo cha Uhandisi wa Usalama kwenye Google jijini Munich ni kitovu cha kimataifa cha uhandisi wa faragha na usalama. Wahandisi Wieland Holfelder na Stephan Micklitz wanafafanua jinsi Google huweka uwazi na udhibiti kwenye bidhaa zake.
Wieland Holfelder alikuwa akiishi Marekani alipopokea barua yake ya kukubaliwa kufanya kazi Google. Alikuwa amehamia Silicon Valley kutoka Ujerumani na alikuwa amefanya kazi huko kwa miaka 12, katika kampuni nyingi ikiwa ni pamoja na Mercedes-Benz. Mwaka wa 2008, kila kitu kilibadilika. Wafanyakazi wenze na marafiki wa Holfelder Wamarekani walifurahia mwajiri na kazi yake mpya. Lakini mahali pake pa kazi baadaye hapakuwa Mountain View, California – palikuwa jijini Munich, Ujerumani. Huko, habari zake hazikupokelewa kwa shangwe sana. Pamoja na ujumbe wa kawaida wa pongezi, Holfelder hakupokelewa kwa ukarimu na furaha kutoka kwa marafiki wake wa Kijerumani alipotaja jina “Google.” Lakini Holfelder anafahamu jinsi Watu wa Ulaya – hasa Wajerumani – walivyo makini kuhusiana na suala la data yao.
Holfelder, Msimamizi wa Kituo cha Uhandisi cha Google, ameketi katika kantini ya ofisi za jijini Munich, ambayo inafanana na mkahawa, kutokana na mapambo yake ya kupendeza na madirisha yanayoanzia sakafuni hadi darini. Kutokana na vijisehemu vya mazungumzo vinavyoweza kupenyeza kelele za jumla kwenye chumba, ni bayana kuwa Kiingereza ni lugha kuu ya “WanaGoogle” jijini Munich. Na ushawishi wa Silicon Valley haushii hapo – jengo la matofali, ambalo lilifunguliwa mwaka wa 2016, lina studio ya mazoezi ya mwili, duka la kahawa, chumba cha biliadi na maktaba. Takribani wafanyakazi 750 kutoka duniani kote hufanya kazi katika tawi hili, wengi wao ni wasanidi programu. Saa zao za kazi huendelea hadi jioni, kwa sababu mikutano ya video na wafanyakazi wenza walio katika makao makuu ya Google, Mountain View inaweza tu kufanyika kuanzia mapema jioni na kuendelea.
Lengo kuu ni kwa watumiaji kupata uwazi na udhibiti kamili kuhusiana na suala la jinsi data yao inavyotumika
Licha ya hayo, shughuli za Google jijini Munich huonekana kuwa za Kijerumani kabisa – hii inatokana na vitu vingi vya msingi kama vile vyumba vya mikutano vilivyoundwa ili kufanana na stesheni za chini ya ardhi au vyumba vya zamani vya Kibavaria vyenye kuta za mbao. Lakini kwa Holfelder, faida kuu ya Kijerumani anayoona kutokana na eneo la kazi kuwa lilipo ni kile anachokiita “fursa yetu ya ndani”: wahandisi wake jijini Munich. “Hapa jijini Munich,” anaelezea Holfelder, “tunabuni huduma na bidhaa za Google – kwa watumiaji duniani kote – katika sehemu ya faragha ya data.” Lengo kuu ni kwa watumiaji kupata uwazi na udhibiti kamili kuhusiana na suala la jinsi data yao inavyotumika. Ujerumani ni eneo mwafaka kwa watu kushughulikia kazi hii.
Mkurugenzi wa Uhandisi Stephan Micklitz, anayesimamia viwango vya faragha ya data katika bidhaa za Google duniani kote, anafanya kazi pia katika ofisi jijini Munich. Baada ya kujiunga na timu mwaka wa 2007, ni mmoja wa WanaGoogle wa kwanza jijini Munich. Ni Micklitz na timu yake waliobuni huduma halisi ya Akaunti Yangu, ambayo baadaye ilibadilika kuwa Akaunti ya Google. Kituo hiki cha dijitali kinaweza kutumiwa na mtu yeyote ambaye ana akaunti ya Google, wakiwemo wale wanaotumia tu mtambo wa kutafuta kwenye Google au YouTube. Akaunti ya Google hurahisisha kudhibiti mipangilio. Watumiaji wanaweza pia kutekeleza Ukaguzi wa Usalama ili kuona jinsi data yao inavyolindwa dhidi ya shambulizi la nje na kutumia Ukaguzi wa Faragha ili kubainisha taarifa zao binafsi ambazo wangependa zihifadhiwe kwenye seva za Google na ambazo hawangependa zihifadhiwe.
"Hapa jijini Munich, tunabuni huduma na bidhaa za Google – kwa watumiaji duniani kote – katika kipengele cha faragha ya data."
Wieland Holfelder
“Tulikuwa na wazo la kuanzisha kitovu kikuu cha maswali yote ya aina hii,” anasema Micklitz. “Tulitaka kuweka majibu yote kwenye kurasa mbili, pamoja na chaguo zote za kuweka mipangilio – lakini kwa kulenga hatua muhimu zaidi, ili tusiwachoshe watumiaji.” Micklitz ameleta kahawa hivi sasa kutoka kwenye mojawapo ya vyumba vidogo vya wafanyakazi wa Google vya kupikia, vinavyojulikana kama “jiko dogo,” ambapo friji yenye kimo cha futi sita imejazwa kabisa vinywaji. Milango ya vioo inatoa mwonekano dhahiri wa safu mbili za juu, ambazo zimejazwa kwa maji ya madini. Vitu vingine vilivyomo kwenye friji vimefichwa nyuma ya kioo kilichoganda. Vinywaji vimepangwa kuanzia juisi zilizohifadhiwa kwa hewa ya kaboni, kisha juisi za kawaida, hatimaye chai za barafu na vinywaji vya kaboni ambavyo havifai kwa afya kwenye rafu za chini. “Sisi wahandisi hatupendi kubahatisha mambo,” anasema Micklitz.
Kulingana na Holfelder na Micklitz, hakuna kampuni nyingine yoyote kwenye sekta inayojitahidi zaidi ya Google katika kulinda data ya watumiaji wake dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni. Ni kweli kuwa mfumo wa seva ya Google unatambuliwa kuwa mojawapo ya mfumo salama zaidi duniani. Mfumo huu wa usalama ni changamano na una viwango vingi. Data huhifadhiwa katika muundo uliosimbwa kwa njia fiche kwenye vituo vya data duniani kote – majengo ambayo yanafanana na magereza ya ulinzi wa hali ya juu. “Hata kama mtu fulani kwenye mojawapo ya vituo vyetu vya data vinavyolindwa kibayometriki atapata diski kuu iliyo na barua pepe zako, hataweza kuitumia kufanya kitu chochote,” anafafanua Holfelder. “Taarifa zote zilizomo husambazwa kwenye vituo mbalimbali vya data – na husimbwa kwa njia fiche.” Pia, ikiwa wadukuzi watagundua udhaifu kwenye bidhaa au violesura vya Google licha ya mbinu hizi zote, kampuni hutoa zawadi maalum ili kupata maelezo hayo. Kwa hivyo, kuna faida kwa wanaotarajia kufanya uhalifu mtandaoni kuripoti udhaifu wa usalama kuliko kutumia fursa hiyo vibaya.
"Tulikuwa na wazo la kuanzisha kitovu kikuu cha maswali yote yanayohusiana na faragha na usalama."
Stephan Micklitz
Kuna hoja mbili muhimu hasa za kutilia maanani kutoka kwenye mazungumzo ya Holfelder na Micklitz. Kwanza, mtu yeyote anayefungua akaunti ya barua pepe au kupakia picha kwenye wingu kwa kutumia Google, anapaswa kufahamu kuwa ujumbe na picha zake zote zimelindwa kadri iwezekanavyo. Pili, mtu yeyote anayetumia Google kufanya utafutaji na kuvinjari mtandaoni anaweza kubainisha mwenyewe data ambayo Google inaruhusiwa kukusanya na kutumia. “Binafsi, mimi hufurahia wakati simu inanipa taarifa za hali ilivyo barabarani na kunieleza, kwa mfano, kuwa ninapaswa kuondoka sasa ikiwa ninataka kufika kwenye uwanja wa ndege kwa wakati kwa sababu kuna msongamano kwenye barabara kuu,” anasema Holfelder. “Lakini kila mtu anaweza kuamua mwenyewe ikiwa angependa kuwasha kipengele hiki au la.”
Hali hiyo pia inatumika kwa matangazo, ambayo ni njia kuu inayotumiwa na Google kujitengenezea pesa. Data inaweza kusaidia kufanya matangazo yakufae zaidi -- kwa hivyo, ikiwa unatafuta sofa mpya ya kijivu, utaonyeshwa matangazo yanayolingana na mahitaji yako. Baadhi watu hunufaika; wengine hukerwa. Micklitz anafafanua kuwa inawezekana kuzima kipengele hiki cha kuweka mapendeleo ya matangazo. “Kupitia Akaunti ya Google, bila shaka,” anaongeza kusema. Watumiaji wanaozima kipengele hiki bado wataonyeshwa matangazo, lakini hayataonyeshwa kulingana na mambo yanayowavutia. “Tunatumia data ili kufanya matangazo yawafae watumiaji wetu,” Holfelder anachangia. “Lakini hatuuzi data yoyote binafsi.”
Picha: Myrzik na Jarisch
Uboreshaji wa usalama mtandaoni
Pata maelezo kuhusu jinsi tunavyohakikisha usalama wa watu wengi zaidi mtandaoni kuliko shirika lolote lingine duniani.
Pata maelezo zaidi