Zana na vidokezo vya kukusaidia
uwe salama mtandaoni.
Tunalinda faragha yako kiotomatiki kwa kutumia mbinu bora zaidi za usalama. Kuna hatua chache za ziada unazoweza kuchukua ili udhibiti usalama wako mtandaoni na uchague kiwango sahihi cha ulinzi unaokufaa.
Ukaguzi wa Usalama
Kagua Usalama
Njia rahisi ya kulinda Akaunti yako ya Google ni kufanya Ukaguzi wa Usalama. Zana hii ya hatua kwa hatua inakupatia mapendekezo mahususi yanayokufaa, yenye hatua unazoweza kuchukua ili uimarishe usalama wa Akaunti yako ya Google.
UTHIBITISHAJI WA HATUA MBILI
Jilinde dhidi ya wadukuzi ukitumia Uthibitishaji wa Hatua Mbili
Uthibitishaji wa Hatua Mbili husaidia kumzuia mtu yeyote ambaye hastahili kufikia akaunti yako kwa kukuomba utumie njia ya pili kando na jina la mtumiaji na nenosiri ili kuingia katika akaunti. Kwa watu walio katika hatari ya kulengwa na mashambulizi mahususi ya mtandaoni na wanahitaji ulinzi thabiti zaidi, tumebuni Mpango wa Ulinzi wa Hali ya Juu.
ulinzi wa manenosiri yako.
Tumia manenosiri thabiti na ya kipekee
Kutunga nenosiri thabiti na maalum kwa kila akaunti ni mojawapo ya hatua muhimu zaidi unayoweza kuchukua ili kulinda faragha yako. Hatua ya kutumia nenosiri lile lile kuingia katika akaunti nyingi, kama vile akaunti ya Google, wasifu wa mitandao jamii na tovuti za wauzaji, huhatarisha usalama.
Fuatilia manenosiri yako yote
Kidhibiti cha manenosiri kama kile kilichojumuishwa kwenye Akaunti yako ya Google, husaidia kulinda na kufuatilia manenosiri unayotumia kwenye tovuti na programu. Kidhibiti cha Manenosiri cha Google kinakusaidia kutunga, kukumbuka na kuhifadhi manenosiri yako yote kwa usalama ili uweze kuingia katika akaunti zako kwa njia rahisi na salama.
Kagua manenosiri yako ili uone kama kuna matatizo ya usalama
Kagua uthabiti na usalama wa manenosiri yako yote uliyohifadhi kwa kufanya Ukaguzi wa Manenosiri kwa haraka. Fahamu iwapo manenosiri yako yoyote uliyohifadhi ya akaunti au tovuti za wengine yameathiriwa na uyabadilishe kwa urahisi panapohitajika.
-
Funga simu yako ikipotea
Ukipoteza simu yako au ikiibwa, unaweza kutembelea Akaunti yako ya Google na uchague “Tafuta simu yako” ili ulinde data yako kwa kufuata hatua chache za haraka. Iwe una kifaa kinachotumia iOS au Android, unaweza kutambua mahali simu yako ilipo na kuifunga kutoka mbali ili mtu yeyote asiitumie wala kufikia taarifa yako ya binafsi.
-
Sasisha programu yako kila wakati
Kagua programu unayotumia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa unatumia toleo jipya zaidi. Baadhi ya huduma, ikiwa ni pamoja na kivinjari cha Chrome, zinaweza kujisasisha kiotomatiki ili upate marekebisho na vipengele vipya zaidi vya usalama.
-
Zuia programu zinazoweza kudhuru zisifikie simu yako
Tunatunza kifaa chako kwa kutumia Google Play Protect, ulinzi uliojumuishwa wa Google dhidi ya programu hasidi kwa ajili ya Android, lakini kila wakati, unapaswa kupakua programu za kifaa chako cha mkononi kutoka chanzo unachoamini. Ili ulinde data yako, kagua programu zako na ufute zile ambazo huzitumii, washa masasisho ya programu ya kiotomatiki na udhibiti uwezo wa programu kufikia data yako nyeti kama vile picha na mahali uliko.
-
Tumia kipengele cha kufunga skrini
Wakati hutumii kifaa chako kiwe kompyuta, kompyuta ya kupakata, kompyuta kibao au simu, funga skrini yake ili uwazuia watu wengine wasikitumie. Ili kuimarisha usalama, weka mipangilio inayoruhusu kifaa chako kujifunga kiotomatiki wakati kiko katika hali tuli.
-
Tumia mitandao salama
Tahadhari kuhusu kutumia Wi-Fi ya umma au isiyolipishwa, hata kama inahitaji uweke nenosiri. Mitandao hii huenda haijasimbwa kwa njia fiche, kwa hivyo unapounganisha kwenye mtandao wa umma, mtu yeyote aliye karibu anaweza kufuatilia shughuli zako kwenye intaneti, kama vile tovuti unazotembelea na maelezo unayoweka kwenye tovuti mbalimbali. Ikiwa huna mtandao mwingine isipokuwa Wi-Fi ya umma au isiyolipishwa, kivinjari cha Chrome kitakujulisha katika sehemu ya anwani ikiwa muunganisho wako kwenye tovuti Si salama.
Tazama video hii ili upate maelezo zaidi kuhusu umuhimu wa kutumia miunganisho salama ya Wi-Fi na upate vidokezo kuhusu jinsi ya kulinda usalama wa mtandao wako wa Wi-Fi.
-
Hakikisha muunganisho wako ni salama kabla ya kuweka taarifa nyeti
Unapovinjari wavuti, hasa unapotaka kuweka maelezo nyeti kama vile nenosiri au namba ya kadi ya malipo, hakikisha muunganisho wa tovuti unazotembelea ni salama. Hali chaguomsingi ya muunganisho wowote ni salama. Ikiwa muunganisho si salama, kivinjari cha Chrome kitaonyesha chipu nyekundu ya "Si Salama" katika sehemu ya anwani. HTTPS husaidia kuimarisha usalama wa shughuli zako za kuvinjari kwa kuunganisha kivinjari au programu zako kwa njia salama kwenye tovuti unazotembelea.
-
Usahihi wa Kipengele cha Google cha Kutambua Mahali
Usahihi wa Kipengele cha Google cha Kutambua Mahali hutumia data ya Wi-Fi ya umma kutoka kwenye milango ya mitandao pasiwaya na GPS, minara ya mtandao wa simu na data ya vitambuzi ili kuboresha huduma za mahali. Kwa maagizo kuhusu jinsi ya kuondoa mlango wa mtandao wako wa Wi-Fi ili usitambuliwe, pata maelezo zaidi hapa.
majaribio ya wizi wa data binafsi
Fahamu jinsi unavyoweza kulaghaiwa
Walaghai hutumia fursa ya nia njema kwa kufanya ulaghai wao uonekane kama ujumbe halali. Kando na barua pepe, walaghai wanaweza pia kutumia ujumbe wa maandishi, simu zinazopigwa kiotomatiki na tovuti hasidi ili kukulaghai.
Thibitisha kila wakati viungo au URL unazotilia shaka
Wizi wa data binafsi ni jaribio la kukuhadaa ili utoe taarifa muhimu ya binafsi au ya kifedha, kama vile nenosiri au maelezo ya benki. Unaweza kutekelezwa kwa njia nyingi, kama vile ukurasa bandia wa kuingia katika akaunti. Ili kuepuka wizi wa data binafsi, usiwahi kubofya viungo unavyotilia shaka; hakikisha usalama wa URL — kwa kufanya kiashiria chako kielee juu ya kiungo au kubonyeza kwa muda mrefu maandishi yaliyo kwenye kifaa chako cha mkononi — ili uhakikishe kuwa programu au tovuti ni halali; na uhakikishe kuwa URL inaanza kwa “https.”
Tahadhari dhidi ya waigaji
Walaghai wanaweza kujifanya kuwa mashirika halali kama vile serikali au mashirika yasiyo ya faida. Tahadhari kila wakati unaposoma ujumbe kutoka kwa mtu anayedai kuwa ana mamlaka fulani. Ikiwa mtu unayemjua atakutumia barua pepe, lakini ujumbe huo uwe si wa kawaida, inamaanisha kuwa huenda akaunti yake imedukuliwa. Usijibu ujumbe au ubofye viungo vyovyote isipokuwa uwe unaweza kuthibitisha kuwa barua pepe ni halali. Chunguza vitu kama vile maombi ya dharura ya pesa, habari za kusikitisha kuwa mtu anateseka ughaibuni na anahitaji usaidizi au mtu anayedai kuwa simu yake imeibwa na hawezi kupatikana kwenye simu.
Tahadhari dhidi ya ulaghai kupitia barua au maombi ya taarifa binafsi
Ujumbe kutoka kwa watu usiowajua unaweza kushukiwa na hata mawasiliano kutoka kwa mtu unayemwani, kama vile benki yako, yanaweza kuwa uigaji. Usijibu barua pepe, ujumbe wa papo hapo au madirisha ibukizi unayotilia shaka, ambayo yanakuomba taarifa binafsi. Usiwahi kubofya viungo unavyotilia shaka au kuweka taarifa binafsi kwenye utafiti au fomu unazoshuku. Ukiombwa utoe msaada kwa shirika lisilo la faida, nenda moja kwa moja kwenye tovuti ya shirika hilo ili utoe mchango wako badala ya kubofya kiungo ulichotumiwa.
Thibitisha faili kabla ya kuzipakua
Baadhi ya wizi wa data binafsi unaweza kutokea kupitia viambatisho vya PDF na hati zilizoathiriwa. Ukipata kiambatisho unachotilia shaka, tumia Chrome au Google Drive kukifungua. Tutachanganua moja kwa moja faili hiyo na kukuonya tukitambua kuwa ina virusi.
kulinda usalama wako mtandaoni.
-
Usalama uliojumuishwaPata maelezo zaidi kuhusu mbinu zetu za ulinzi wa kiotomatiki.
-
Vidhibiti vya faraghaChagua mipangilio ya faragha inayokufaa.
-
Kanuni za dataPata maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyoheshimu faragha yako kwa kutumia kanuni za data.
-
Matangazo na dataPata maelezo zaidi kuhusu matangazo unayoonyeshwa kwenye mifumo yetu.