Taarifa na maudhui

unayoweza kuyaamini.

Hapa Google, tunalenga kusawazisha kati ya maelezo tunayotoa na kuwalinda watumiaji na jamii. Tunachukulia wajibu huu kwa uzito. Lengo letu ni kutoa ufikiaji wa taarifa na maudhui yanayoaminika kwa kuwalinda watumiaji dhidi ya hatari, kuwasilisha taarifa zinazoaminika na kushirikiana na wataalamu na mashirika ili kuimarisha zaidi usalama wa intaneti.

Kukulinda dhidi ya hatari.

Tunaimarisha usalama wako na wa jamii kwa ujumla kwa kutumia mipangilio ya ulinzi wa hali ya juu ambayo haizuii tu, lakini pia inatambua na kushughulikia maudhui hatari na yanayokiuka sheria.

Kuzuia

Kuzuia matumizi mabaya

Ili kuimarisha usalama wa watumiaji dhidi ya maudhui mabaya, tunatumia mbinu za ulinzi zilizowezeshwa kwa AI. Gmail inazuia kiotomatiki takribani barua pepe taka milioni 10 kwenye vikasha kila dakika na huduma ya Tafuta ina zana za kuzuia kipengele cha Kukamilisha kiotomatiki kisipendekeze hoja zinazoweza kuwa hatari. Utambuzi wa kiotomatiki husaidia YouTube kuondoa maudhui hatari kwa ufanisi, ipasavyo na kwa kiwango kikubwa. Katika robo ya pili ya mwaka 2023, asilimia 93 ya video zilizoondolewa kwenye YouTube kwa kukiuka sera zilitambuliwa mara ya kwanza kiotomatiki. Tunatumia pia mbinu za usalama kwenye zana zetu za AI zalishi ili kupunguza hatari ya zana hizo kutumiwa kutayarisha maudhui hatari.

Pamoja na hayo, kila bidhaa yetu inasimamiwa na mkusanyiko wa sera zinazobainisha tabia na maudhui yanayokubalika na yasiyokubalika. Sera zetu zinaboreshwa na kusasishwa kila mara ili kushughulikia hatari zinazoibuka. Katika suala la utumiaji wetu wa AI, tunategemea pia Kanuni zetu za AI ili kuongoza mchakato wa utayarishaji wa bidhaa na kutusaidia kujaribu na kutathmini kila programu ya AI kabla ya kuzinduliwa.

Kutambua

Kutambua maudhui hatari

Kadiri mbinu za watendaji wabaya zinavyobadilika, ni lazima tujitahidi zaidi ili kutambua maudhui hatari yanayochapishwa kwenye bidhaa zetu. Zana za AI zinatusaidia kuimarisha utambuzi wa matumizi mabaya kwenye mifumo yetu. Viainishi vinavyowezeshwa na AI husaidia kuripoti kwa haraka maudhui ambayo huenda yakawa hatari ili yaondolewe au yaelekezwe kwa mhakiki mwanadamu. Mwaka 2022, utekelezaji wa kiotomatiki ulitusaidia kutambua na kuzuia zaidi ya matangazo milioni 51.2 yenye matamshi ya chuki, vurugu na madai hatari ya afya. Pamoja na hayo, Mifumo Mikubwa ya Lugha, ambayo ni aina muhimu ya AI, inaonyesha uwezekano wa kupunguza kwa kiasi kikubwa muda unaotumika kutambua na kutathmini maudhui hatari, hususani yanayotokana na hatari mpya na zinazoibuka.

Pia tunashirikiana na mashirika ya nje, ambayo huripoti maudhui wanayofikiria yanaweza kuwa hatari. Google na YouTube hupokea maoni kutoka kwa mamia ya Wapigaripoti Wanaopewa Kipaumbele, mashirika kutoka kote ulimwenguni yenye wataalamu wa maudhui na utamaduni ambao huelekeza maudhui kwetu ili tuyakague.

Kushughulikia

Kushughulikia ipasavyo

Tunategemea watu na teknolojia inayotumia AI kutathmini ukiukaji wa sera unaoweza kutokea na kushughulikia ipasavyo maudhui yanayoripotiwa. Maudhui yanapokiuka sera zetu, tunaweza kuyazuia, kuyaondoa, kukomesha uchumaji wa mapato au kuchukua hatua katika kiwango cha akaunti ili kupunguza matumizi mabaya katika siku zijazo.

Mwaka 2022, huduma ya Ramani za Google ilizuia au kuondoa zaidi ya vipande milioni 300 vya maudhui bandia, maoni milioni 115 yanayokiuka sera na majaribio milioni 20 ya kufungua Wasifu bandia wa Biashara. Katika robo ya pili ya mwaka 2023, YouTube iliondoa zaidi ya chaneli milioni 14 na video milioni 7 kwa kukiuka Mwongozo wetu wa Jumuiya.

Ili kutathmini muktadha na hali, huku tukipunguza hatari ya kuondoa maudhui kupita kiasi, tunategemea takribani wahakiki elfu 20 wa kitaalamu waliohitimu kufanya kazi katika majukumu mbalimbali ili kutekeleza sera zetu, kudhibiti maudhui na kutathmini maudhui yanayoripotiwa kwenye bidhaa na huduma za Google.

Ikiwa mtayarishi au mchapishaji anahisi tumefanya maamuzi yasiyo sahihi, anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi wetu.

Kuwasilisha maelezo ya kutegemeka.

Tunahakikisha maudhui na maelezo yaliyo kwenye mifumo yetu yanaaminika kwa kutoa maelezo ya kutegemeka na zana bora zaidi zinazokuwezesha kutathmini maudhui kwa usahihi.

Jinsi tunavyopanga maelezo

Algoriti mahiri

Algoriti zetu zinazosasishwa mara kwa mara ni sehemu muhimu ya kila tunachofanya, iwe ni kwenye bidhaa kama vile Ramani za Google au Matokeo ya utafutaji. Algoriti hizi zinatumia Mifumo Mikubwa ya Lugha iliyoboreshwa na viashiria kama vile maneno muhimu au upya wa maudhui na tovuti ili uweze kupata matokeo muhimu na yanayofaa zaidi. Kwa mfano, YouTube huonyesha kwa udhahiri maudhui yenye ubora wa juu kutoka kwenye vyanzo vinavyoaminika katika vidirisha vya matokeo ya utafutaji, mapendekezo na maelezo ili kuwasaidia watu kupata habari na taarifa muhimu, sahihi na za wakati unaofaa.

Zana za kukusaidia kutathmini maudhui

Tumebuni vipengele kadhaa vya kukusaidia kuelewa na kutathmini maudhui ambayo algoriti na zana zetu za AI zalishi zimeangazia, ili kuhakikisha kwamba unaelewa zaidi kuhusu maudhui unayoyaona mtandaoni.

Kudhibiti Maudhui kwa Uwajibikaji kwenye YouTube

YouTube imejitolea kukuza mfumo unaowajibika ambao unaweza kutegemewa na watazamaji, watayarishi na watangazaji katika jumuiya yetu.
Pata maelezo zaidi kuhusu mbinu zetu.

Kushirikiana kukuza intaneti salama zaidi.

Tunazidi kushirikiana, kuarifu na kuruhusu wataalamu na mashirika yafikie zana na teknolojia zetu.

Kubadilishana Maarifa

Kubadilishana maarifa ili kuimarisha usalama wako

Tunashirikiana na wataalamu kutoka mashirika ya kiraia, wanataaluma na serikali ili kushughulikia masuala ya kimataifa kama vile maelezo ya kupotosha, usalama wa matangazo, uadilifu katika uchaguzi, AI kwenye udhibiti wa maudhui na kupambana na unyanyasaji wa watoto mtandaoni. Pia, tunachapisha matokeo ya utafiti na kutoa seti za data kwa wasomi ili kuendeleza uchambuzi na uelewa wa suala hili.

Kwenye YouTube, tunawasiliana mara kwa mara na Kamati yetu huru ya Ushauri ya Vijana na Familia kuhusu masasisho ya bidhaa na sera, ikijumuisha Kanuni zetu za Kuwalinda Vijana, pamoja na mfululizo wa masasisho ya bidhaa yanayoangazia afya ya akili na siha ya vijana.

Kutumiana Viashiria

Kushirikiana na wataalamu ili kupambana na maudhui yanayokiuka sheria

Pia, tunashirikiana na washirika ili kufichua na kutuma viashiria vya wazi vya maudhui mabaya ili kuruhusu yaondolewe kwenye mfumo mpana. Kila mwaka, tunatuma mamilioni ya viwakilishi vya Maudhui yanayoonyesha unyanyasaji wa watoto kingono (CSAM) kwa Kituo cha Kitaifa cha Watoto Waliopotea na Wanaonyanyaswa. Pia, tunashiriki kwenye Project Lantern, mpango unaowezesha kampuni za teknolojia kutumiana viashiria katika njia salama na ya uwajibikaji. Pamoja na hayo, YouTube ilihusika katika kuanzisha Jukwaa la Mtandaoni la Kimataifa la Kukabili Ugaidi (GIFCT), ambalo huwaleta pamoja wadau kutoka sekta ya teknolojia, serikali, mashirika ya kiraia na wanataaluma ili kukabiliana na shughuli za magaidi na wanaosababisha vurugu za itikadi kali mtandaoni.

Kugawana Nyenzo

Kusaidia mashirika yanayojikita katika masuala ya usalama

Tunatoa usaidizi kwa mashirika kote ulimwenguni ambayo yanajikita katika masuala ya usalama wa mtandaoni na ufahamu kuhusu habari kupitia programu madhubuti zinazotoa mafunzo na nyenzo, kama vile Be Internet Awesome, Hit Pause kwenye YouTube na Google News Lab. Pia, Google na YouTube zilitangaza ruzuku ya dola milioni 13.2 kwa Mtandao wa Kimataifa wa Kuhakikisha Ukweli (IFCN) ili kusaidia mtandao wake wa mashirika 135 ya kuhakikisha ukweli. Kwa pamoja, ushirikiano wetu umewezesha zaidi ya wanahabari elfu 550 kupata ujuzi wa uthibitishaji wa kidijitali na tumewapa mafunzo wengine milioni 2.6 mtandaoni.

Kuruhusu ufikiaji wa API za Usalama

Tunaruhusu mashirika mengine yafikie zana zinazoyasaidia kulinda mifumo na watumiaji wao dhidi ya maudhui hatari.

GSEC DUBLIN

Kushughulikia suala la Uwajibikaji wa maudhui jijini Dublin

Kituo chetu cha Uhandisi wa Usalama kwenye Google cha Uwajibikaji wa Maudhui jijini Dublin ni kituo cha kikanda cha wataalamu wa Google wanaojitahidi kupambana na ueneaji wa maudhui hatari na yanayokiuka sheria. Pia, ni mahali ambapo tunaweza kuruhusu kazi hii ifikiwe na watunzi wa sera, watafiti na wadhibiti. Mtandao wetu wa Vituo vya Uhandisi wa Usalama kwenye Google unazipa timu zetu fursa, hamasa na usaidizi ili kubuni nyenzo mpya za kusaidia kuboresha usalama mtandaoni.

Hali salama zaidi inayofaa ya utumiaji wa intaneti — kimuundo.

Juhudi zetu za kutoa maudhui na maelezo ya kuaminika ni muhimu sana. Ili kuendana na changamoto mpya za kudhibiti maudhui, tutaendelea kuwekeza katika kubuni na kuboresha sera, bidhaa na michakato inayokusaidia kuondoa wasiwasi na kutengeneza hali salama zaidi ya utumiaji wa mtandao kwa wote.

Gundua jinsi Google husaidia
kuhakikisha usalama wa kila mtu mtandaoni.