Njia rahisi na salama zaidi ya kuingia katika akaunti zako bila nenosiri
Funguo za siri ni njia salama na rahisi zaidi ambayo hutumika badala ya manenosiri. Zinakuruhusu uingie katika akaunti ukitumia tu alama ya kidole, uchanganuzi wa uso au kipengele cha kufunga skrini. Pata maelezo zaidi kwa kupakua PDF yetu ya maelezo ya ukurasa mmoja.
Tulisaidia kusanidi funguo za siri kama wanachama wa FIDO Alliance, muungano wa sekta huria uliojitolea kusaidia kupunguza utegemezi wa manenosiri, kurahisisha michakato ya kuingia katika akaunti na kuifanya Intaneti kuwa salama zaidi.
Funguo za siri ni rahisi mara 4 zaidi kutumia kwa kuwa hazihitaji kukumbukwa au kuandikwa. Unatumia tu alama ya kidole, uchanganuzi wa uso au kipengele cha kufunga skrini kuingia katika akaunti kwenye vifaa na mifumo yako yote.
Funguo za siri hukupa ulinzi thabiti zaidi dhidi ya hatari kama vile wizi wa data binafsi. Na kwa kuwa zinahifadhiwa kwenye kifaa chako, haziwezi kukisiwa au kutumiwa tena kwa hivyo zinaimarisha usalama wa maelezo yako dhidi ya wavamizi.
Ufunguo wako wa siri hubaki kuwa wa faragha kwenye kifaa chako binafsi na kamwe haufikiwi na Google au washirika wengine wowote. Unatumia tu alama yako ya kidole, uchanganuzi wa uso au kipengele cha kufunga skrini ili uthibitishe kuwa ni wewe unayefikia ufunguo wako binafsi.
Funguo za siri hutoa hali salama na rahisi zaidi ya kuingia katika akaunti kwa watumiaji wote walio na akaunti binafsi za Google, zaidi ya wateja milioni 9 wa Google Workspace na programu za wengine.
Kuleta funguo za siri kwenye biashara na serikali
Funguo za siri huwapa watumiaji manufaa muhimu ya usalama na urahisi wa kutumia na tunafurahi kuwa wa kwanza kuwaletea wateja wetu teknolojia hii kati ya watoaji wakuu wa huduma za wingu kwa umma. Mbinu hii inaweza kutumiwa na biashara ndogo na kubwa na pia shuleni na serikalini.
Kushirikiana katika matumizi ya mbinu salama ya kuingia katika akaunti bila nenosiri kwenye mifumo mbalimbali ya Intaneti
Tunashirikiana na chapa ili kuruhusu matumizi ya funguo za siri kwenye mifumo mbalimbali ya Chrome na Android na kuanzisha mbinu za kuingia katika akaunti ambazo ni rahisi na salama kwa watumiaji wao. Washirika katika sekta za usafiri, biashara za mtandaoni na teknolojia ya fedha pamoja na watoa huduma wengine wa programu tayari wamejiunga nasi katika safari yetu ya kutotumia manenosiri.
Je, ufunguo wa siri utachukua kabisa nafasi ya nenosiri?
Maono yetu ni kuwa na mustakabali usio na manenosiri kwa kuwa funguo za siri hufanya iwe rahisi na salama zaidi kuingia katika akaunti. Tunapofanya mabadiliko haya, manenosiri bado yatapatikana na unaweza kuyatumia wakati wowote unapotaka.
Je, bado ninaweza kutumia nenosiri langu kuingia katika akaunti baada ya kujiandikisha kwenye kipengele cha ufunguo wa siri?
Ndiyo, unaweza kuingia katika akaunti ukitumia nenosiri lako na uthibitishaji wa hatua mbili, ikiwa umeweka mipangilio hiyo. Ukiwa na ufunguo wa siri, unapata uwezo wa kuingia katika akaunti haraka zaidi badala ya kutumia nenosiri na mbinu yako ya uthibitishaji wa hatua mbili.
Je, ninahitaji kuweka mipangilio ya ufunguo wa siri kwenye vifaa vyangu vyote mahususi? Je, kutakuwa na funguo tofauti za siri kwenye simu na kompyuta yangu ya kupakata?
Ikiwa Google itatambua kuwa bado huna ufunguo wa siri kwenye kifaa, tutakuomba uweke mmoja. Utahitaji ufunguo mmoja wa siri kwa kila kifaa, isipokuwa kama kifaa tayari kina mbinu fulani ya "kusawazisha" funguo za siri kwenye vifaa vingine, kama vile Apple iCloud. Katika hali hii, utahitaji tu ufunguo mmoja wa siri kwenye vifaa vyako vyote vya iCloud.
Ikiwa ninajaribu kuingia katika akaunti kwenye kifaa kipya (kama vile kompyuta katika maktaba) na sina simu yangu ya kuniwezesha kuingia katika akaunti kupitia ufunguo wa siri, je, kuna njia nyingine yoyote ninayoweza kutumia kuingia katika akaunti?
Ndiyo, unaweza kuingia katika akaunti ukitumia njia yako ya kawaida, ambayo mara nyingi huwa ni kutumia jina la mtumiaji na nenosiri lako.
Je, nitafuata taratibu zipi kurejesha uwezo wa kufikia akaunti ikiwa nimeondolewa na sina simu yangu, tuseme imepotea au imeharibika na siwezi kuthibitisha utambulisho wangu?
Unaweza kurejea wakati wowote kwenye chaguo za awali za uthibitishaji kama vile manenosiri na uthibitishaji wa kawaida wa hatua mbili. Katika hali ambapo hukumbuki tena nenosiri lako, unaweza pia kupitia utaratibu wa Google wa kurejesha uwezo wa kufikia Akaunti. Tunakuhimiza uweke anwani ya barua pepe na namba yako ya simu ili uhakikishe kuwa unaweza kufikia akaunti yako kila wakati.
Je, nitahitaji kuweka mipangilio ya ufunguo wa siri katika programu nyinginezo kando kando ikiwa zimeunganishwa kwenye Akaunti yangu ya Google?
Ikiwa unatumia kipengele cha “Ingia ukitumia akaunti ya Google”, basi hapana. Unahitaji tu ufunguo wa siri ili uweze kuingia katika Akaunti yako ya Google. Ikiwa unatumia njia ya moja kwa moja "inayotegemea nenosiri" kuingia katika akaunti kwenye tovuti, huduma au programu leo, kuna uwezekano kwamba utapewa fursa ya kuweka ufunguo tofauti wa siri kwenye huduma hiyo wakati mwingine utakapoingia katika akaunti, ikiwa huduma hiyo inaruhusu matumizi ya funguo za siri.
Je, ufunguo wa siri unatofautiana vipi na funguo za usalama za maunzi?
Funguo za siri zinaweza kuhifadhiwa katika ufunguo halisi wa usalama au kwenye kifaa chako cha kuchakata data (simu, kompyuta binafsi, Mac n.k). Kwa miaka mingi, mahali pekee ambapo watumiaji wangeweza kuhifadhi funguo za siri palikuwa kwenye funguo halisi za usalama. Sasa, ili kurahisisha mambo, unaweza kupata kiwango kile kile cha ulinzi dhidi ya wizi wa data binafsi unachopata kwenye funguo za siri zilizohifadhiwa katika funguo za usalama, ukitumia funguo za siri ambazo sasa zinahifadhiwa katika simu na vifaa vyako vingine. Hutakiwi kuchukua hatua yoyote tofauti; mambo yamerahisishwa tu. Badala ya kuhitaji ufunguo wa siri ulio kwenye ufunguo wako halisi wa usalama unapoingia katika akaunti, sasa unaweza pia kutumia ufunguo wa siri ulio katika kompyuta ya kupakata au kompyuta yako ya mezani.
Je, ni lazima nijijumuishe katika kipengele cha ufunguo wa siri?
Hapana, unaweza kuamua kuendelea kutumia nenosiri lako kuingia katika akaunti. Hata hivyo, baada ya muda, watumiaji watakavyozidi kuzoea funguo za siri, huenda tukadhibiti sehemu ambazo tunaruhusu manenosiri yatumike kwa sababu yana kiwango cha chini cha usalama kuliko funguo za siri.
kuimarisha usalama wako mtandaoni.
-
Usalama uliojumuishwaPata maelezo zaidi kuhusu mbinu zetu za ulinzi wa kiotomatiki.
-
Vidhibiti vya faraghaChagua mipangilio ya faragha inayokufaa.
-
Kanuni za dataPata maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyoheshimu faragha yako kwa kutumia kanuni za data.
-
Vidokezo vya usalamaGundua vidokezo vya haraka na desturi bora za kuwa salama mtandaoni.